Jumla ya wagonjwa 18 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo katika kambi maalum ya upasuaji inayofanywa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Hospitali ya Saifee ya New Delhi nchini India.
Upasuaji wa moyo unaofanyika katika kambi hiyo ya siku sita ni wa kufungua kifua kwa watu wazima.
Upasuaji utakaofanyika ni wa kupandikiza mishipa ya damu kwenye moyo (CABG – Coronary Artery Bypass Grafting) na kubadili milango miwili hadi mitatu ya moyo (Valve).
Daktari bingwa wa Moyo na mishipa ya damu ambae pia ni Kaimu mkurugenzi wa Idara ya upasuaji wa Moyo Bashir Nyangasa amesema katika kambi hiyo wanatarajia kufanya upasuaji kwa wagonjwa watatu kwa siku
Dkt. Nyangasa amesema changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni wagonjwa wengi wanaowapokea mioyo yao kutokuwa katika hali nzuri na hivyo kuwashauri wananchi kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara.
Aidha Dkt. Nyangasa aliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kuchangia damu kwani wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji wa moyo wanahitaji kuongezewa damu nyingi kati ya chupa 5 hadi 6.