Wizara ya Afya ya Zanzibar imetoa taarifa ya mwenendo wa Corona nchini leo Aprili 28, 2020 ambapo watu 7 ambao ni raia wa Tanzania kutokea Unguja wamekutwa na maambukizi ya Virusi vya Corona.
Visa vya wagonjwa 7 vilivyotajwa leo kuongezeka vimefikisha idadi ya wagonjwa kuwa 105 kutoka 98 ambao walitolewa taarifa tarehe 24 Aprili, 2020.
Wizara imesema imewaruhusu wagonjwa 36 kwenda nyumbani baada ya dalili zao za maradhi kuondoka ikiwemo homa, kikohozi, kifua kubaba na kuumwa kichwa.
mbali na wagonjwa hao kuruhusiwa kutoka wameshauriwa na wataalamu wa Afya kubaki katika nyumba zao kwa muda wa siku 14 na kuahidiwa kuendelea kufuatiliwa kwa karibu na wataalamu hao ili kujionea maendeleo yao pindi wawapo nyumbani.
Serikali ya visiwani humo imewataka wananchi wake kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo wa Corona na pia imewataka wananchi ambao wana dalili za homa kali, kukohoa na kupiga chafya kuweza kujitokeza katika vituo vya afya mapema au kupiga simu namba 190.