Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli leo Machi 16, 2020 amefuta mbio za Mwenge kwa mwaka huu 2020 hadi pale ugonjwa wa corona utakapoisha.
Rais Magufuli amesema ameamua kufuta mbio hizo mwaka huu kwa kuwa zinaleta mkusanyiko wa watu wengi na kutokana na ugonjwa wa corona unaoendelea kuongeza idadi ya wagonjwa kila kukicha na hata kusababisha vifo, kuwepo kwa mbio hizo kutahatarisha maisha ya watanzania wengi.
Kwa mwaka huu mbio za mwenge zilitegemewa kuwashwa Zanzibar hivi karibuni ambapo ungewezwa kutembezwa nchi nzima na kwa kuchukua tahadhari ya ugonjwa huo ni vyema kuchukua tahadhari mapema zakuzuia mikusanyiko.
Rais Magufuli amesema fedha za mwenge ambazo zilipaswa kutumika kuwasha mwenge Zanzibar zitatumika katika kujiandaa na tahadhari zaidi ya corona ambayo kwa sasa tayari imeshafika Kenya na Rwanda.
“Ndugu zangu ugonjwa huu unaua,ugonjwa ushafika kwa majirani zetu ni lazima tuchukue tahadhari utatumaliza”-amesema Rais Magufuli.
Amesema hadi sasa hakuna mgonjwa wa corona hapa nchini na mbio za mwenge zitaendelea itakapothibitishwa ugonjwa huo umeisha duniani.
Aidha, Rais Magufuli ameendelea na ziara katika barabara zinazoendelea na ujenzi wa kupanuliwa ambazo ni za Mwenge, Mbezi na Kimara huku aikisisitiza wananchi kuchukua tahadhari na kuwatahadharisha watanzania kutokugusana na kuepuka misongamano.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi mtendaji wa Wakala wa Barabara (Tanroads), Patrick Mfugale amesema ujenzi wa daraja la Mfugale linalounganisha barabara ya Morogoro, Mandela na Sam Nujoma umefikia zaidi ya asilimia 70.
Patrick amesema ujenzi wa daraja hilo unatumia zaidi ya Shilingi bilioni 200 huku Rais Magufuli akipongeza maendeleo mazuri ya ujenzi wa daraja hilo kwa kusema ameridhishwa na ujenzi huo.
Mwisho.