Maafisa usafirishaji na wafanya biashara wadogo wa kituo cha mabasi Halmashauri ya mji wa Makambako wameiomba halmashauri kuchukua hatua za haraka kufanya ukarabati wa Kituo hicho, ili kuepusha hasara na mlipuko wa magonjwa yanayoweza kujitokeza kutokana na ubovu wa miundombinu ya kituo hicho.
Taarifa na Dickson Kanyika
Madereva hao pamoja na Halmashauri ya mji wa Makambako wamesema hali ya miundombinu ya stendi hiyo hairidhishi wakati wanalipa ushuru kwa mamlaka husika.
Maafisa usafirishaji wanalalama kwamba halii imeendelea kuwapa hasara kutokana na magari yao kuharibika hali inasababisha kukosekana kwa maelewano baina ya madereva na waajiri wao.
Ndani ya Kituo hicho cha mabasi kinaelezwa pia kuwepo na wajasiriamali wadogo ambao wanafanya biashara za uuzaji wa vyakula na vinywaji ambao wamesema hali ya usalama wa afya zao na watumiaji wa bidhaa wanazoziuza ndani ya kituo hicho si salama kutokana na kuwepo kwa maji yaliotuama kwa muda mrefu yanayombatana na Harufu kali.
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya mji huu wa Makambako Rashid Njozi Musa amekiri kuwepo kwa changamoto ya ubovu wa miundombinu, ambapo amesema yeye kama kiongozi wa halmashauri wanashughulikia tatizo hilo na wanasubiri mvua zipungue ili ukarabati uweze kufanyika haraka iwezekanavyo.
Mwisho.