Ndole ni kijiji ambacho kipo pembezoni mwa Wilaya ya Mvomero katika milima ya Ndole, wakazi wa kijiji hicho wengi wao wakijishughulisha zaidi na kilimo cha mazao ya Ndizi, maharage pamoja na magimbi ambayo yamekuwa yakisafirishwa sehemu mbalimbali nchini.
Licha ya kujituma katika uzalishaji wa mazao lakini kwa sasa wanakatishwa tamaa kutokana na adha ya usafiri unaosababishwa na kubomoka kwa daraja linalounganisha kjiji hicho na vijiji jirani hata kupelekea magari kushindwa kutoka au kuingia ndani ya kijiji hicho.
Wafanyabiashara na madereva wa magari nao wanakumbwa na changamoto hiyo ya kubomoka kwa daraja hatua inayowalazimu kuzunguka umbali mrefu kuingia kijijini hapo kupitia Gairo pamoja na Kibati.
Uongozi wa kijiji cha Ndole kupitia kwa Mwenyekiti wa kijiji hicho Adrian Paulo amesema mamlaka husika inayohusika na ujenzi wa miundombinu wamepewa taarifa kuhusu adha hiyo lakini wanashangazwa na ukimya uliopo,
Wakati bado wananchi hao wanasubiri ufumbuzi wa ujenzi wa daraja hilo, vijana wa kijiji hicho watengeneza mfano wa daraja dogo la miti ambalo nalo si salama kutokana na kuhitaji umakini mkubwa wakati wa kupita hasa kwa wale wanaotumia usafiri wa pikipiki.
Licha ya kuwa ni hatari lakini si haba kutokana na mizigo mingi kupitishwa na pikipiki kupitia mfano huo wa daraja hilo, huku magari yayotoea maeneo ya Dumila,Turiani na Morogoro yakiishia ng’ambo na yale yanayotoka kijijini hapo nayo yakiishia ng’ambo ya pili ya mto.
Serikali ya wilaya Mvomero imekirii kutambua uwepo wa changamoto hiyo ya kubomoka kwa daraja inayaokawabili wakazi wa kijiji cha Ndole na wako kwenye mchakato wakulitengeneza.
Kwa mara ya Kwanza Daraja hilo limebomoka mwezi wanne mwaka 2019, ambapo mpaka sasa limejengwa zaidi ya awamu tatu lakini awamu hizo zote limekuwa likibomelewa na mvua na hivyo kupelekea changamoto ya usafiri kusuasua hatua ambayo inatajwa kurudisha nyuma maendeleo ndani ya kijiji hicho kutokana na idadi ya watu wanaoingia kupungua huku wananchi nao wakishindwa kusafirisha mazao yao kwenda sokoni na hivyo kupelekea mazao mengi kuharibika na wengine kuamua kuuza kwa bei ya chini.
Mwisho.