Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ametangaza maombolezo ya kitaifa baada ya kufariki Rais wa pili wa nchi hiyo, Daniel Arap Moi.
Mzee Moi ambaye amefariki asubuhi ya leo hospitali ya Nairobi akiwa amezungukwa na familia yake mpaka sasa ratiba ya mazishi bado haijawekwa hadharani.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu ya Kenya imesema muda wa maombolezo utaisha baada ya mazishi ya Mzee Moi.
Katika kipindi chote cha maombolezo, bendera ya Kenya itapeperushwa nusu mlingoti kwenye majengo na ofisi zote za umma, jeshi na ofisi za ubalozi wa nchi hiyo kote duniani.
Baadhi ya wananchi wa Kenya wametoa salamu zao juu ya kifo cha Rais Moi ambapo miongoni mwao wamesema kwa muda wa miaka 24 ya utawala wa Mzee Moi kutoka 1978 mpaka 2002 ilikuwa ni mchanganyiko wa maendeleo na utawala wa mkono wa chumai.
Taarifa zimeeleza kuwa jeshi la nchini Kenya litaongoza mipango yote ya mazishi ya Amiri Jeshi huyo mstaafu wa nchi hiyo.
Viongozi mbalimbali wametuma salamu zao za rambirambi akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli ameandika katika ukarasa wake wa twitter
"Kwa niaba ya Serikali na Watanzania nakupa pole Mhe.Rais Uhuru Kenyatta na Wakenya wote kwa kuondokewa na Rais Mstaafu Daniel Toroitich arap Moi. Watanzania tutamkumbuka kwa uongozi wake mahiri, jitihada za kuimarisha uhusiano wetu na Kenya na kufufua Jumuiya ya Afrika Mashariki."
Viongozi wengine waliotuma salamu za rambirambi kwa familia ya Rais Moi na nchi ya Kenya ni pamoja na Waziri Mkuu wa Ethiopia pamoja na balozi wa Marekani nchini Kenya Kyle McCarter
Mwisho.