Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi amesema Tanzania inaendelea kufuatilia kwa ukaribu maendeleo na hali za watanzania wanaoishi jimboni Wuhan nchini China kwa ujumla kutokana na kuzuka kwa virusi vya homa ya Corona nchini humo.
Habari na Angela Mathayo.
Prof. Kabudi amesema Tanzania ina wanafunzi takribani 4000 ambapo katika mji wa Wuhan kuna wanafunzi 400 ambapo kwa mujibu wa Balozi wa Tanzania Nchini China Balozi Mbelwa Kairuki ameihakikishia serikali kuwa mpaka sasa hakuna mtanzania yeyote aliyeathiriwa ama kukumbwa na maradhi hayo.
Prof Kabudi amewataka watanzania kuwa watulivu na kupenda kuwa na subira ya kupata maelezo na ufafanuzi rasmi kutoka kwa Serikali pale panakotokea jambo badala ya kukimbilia kwenye mitandao ya kijamii na nakuamini habari hizo za uvumi kwani kwa kufuatilia habari hizo kutoka vyanzo husika vya kutoa habari kutaondoa uenezi wa habari zinazoua taharuki.
Aidha amewataka watanzania kuwa makini na suala la kutoa taarifa zisizo rasmi ama uvumi ambazo hazijathibitishwa kutoka kwa mamlaka husika kwani kwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria za Tanzania na amewasihi wawe na subira wakati wakiendelea kupata taarifa rasmi kutoka serikalini.
Mwisho