Waziri wa elimu, sayansi na teknolojia Profesa Joyce Ndalichako ameamuru Mhandisi mshauri anayesimamia mradi wa ujenzi wa chuo cha elimu na mafunzo ya ufundi stadi VETA mkoa wa Rukwa pamoja na mkandarasi wakamatwe na kuwekwa ndani kwa muda usiojulikana kutokana na kushindwa kukamilisha ujenzi wa chuo hicho kwa wakati licha ya kuongezewa muda.
Taarifa yake;Brown Lawi Mtawa.
Maagizo ya kukamatwa kwa mhandisi mshauri pamoja na mkandarasi wa Tenda Company ltd yametolewa na Prof. Ndalichako baada ya kukagua ujenzi wa chuo cha VETA na kuona ujenzi huo bado unasuasua.
“Kwahiyo akakae ndani mpaka vile vifaa ulivyoruhusu hapa vitakaporudi ndio mumuachie kwasababu naona sasa hii itakuwa ni kuchezeana, majibu yanayoeleweka hakuna unayonipa siwezi kuwa nakuja kila siku natoa maelekezo hayatekelezwi” -Prof.Joyce Ndalichako-Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia
Kwa upande wao baadhi ya wafanyakazi katika chuo hicho wameeleza changamoto wanazokabiliana nazo pindi wanapokuwa katika ujenzi wa chuo hicho cha ufundi.
“Mnaweza mkapangiwa kazi lakini mkimaliza kazi mapema mnaongezewa kazi baada ya kuona kwamba hawa watu hawajachoka hata ikiwa ni saa sita usiku mnapewa elfu sita ileile”-Simon Mateo – Mfanyakazi wa Kibarua Tender company ltd.
Kukamilika kwa chuo hicho cha VETA kutasaidia kuleta mafanikio kwa wakazi wa Rukwa na taifa kwa ujumla katika kuijenga Tanzania ya viwanda kwakuwa kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafuzi zaidi ya 1500 kwa mwaka katika kada tofauti.
Mwisho.