Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam nchini Tanzania imeshindwa kuendelea na kesi inayowakabili viongozi wa Chadema akiwemo Mwenyekiti wake ambaye ni Freeman Mbowe.
Kesi hiyo ambayo ilikuwa iendelee leo Novemba 26, 2019 kwa kuendelea kusikiliza utetezi imeshindwa baada ya wakili wa utetezi kueleza afya ya Mbowe bado sio nzuri.
Wakili wa utetezi, Peter Kibatala amedai mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa afya Mbowe bado sio nzuri kwa kuwa bado anaumwa. Wakili Mkuu wa Serikali, Faraja Nchimbi amedai walipokea taarifa ya mshtakiwa wa kwanza ikiambatanishwa na taarifa ya daktari.
"Mbowe bado anaumwa, ameruhusiwa kutoka hospitali Ijumaa Novemba 22, 2019 na anasumbuliwa na Dengue, shinikizo la juu la damu pamoja na malaria," amesema Kibatala
Alidai kama mshtakiwa aliruhusiwa tangu Ijumaa Novemba 22,2019 na kwa utaalamu wa madaktari ina maana mgonjwa huyo atakuwa amepona.
"Hatuoni sababu ya kuahirisha kesi hii Mahakama ilipanga kusikiliza, kuiahirisha inabidi kuwa na uthibitisho utakaoonyesha sababu ya kuahirisha kama atakuwa ametoka hospitali toka Ijumaa atakuwa kapumzika vya kutosha" amesema Nchimbi
Kesi inayowakabili Mbowe na wenzake ni mashtaka 12 likiwemo shitaka la uchochezi, kufanya mkusanyiko usio halali na kukaidi amri ya jeshi la polisi.