Mbunge wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema, Cecil Mwambe amesema anagombea nafasi ya juu ya chama hicho ili kumsaidia mwenyekiti wa sasa, Freeman Mbowe ….
Mwambe ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema amesema hayo leo Jumanne Novemba 26, 2019 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu adhima ya kugombea nafasi hiyo.
“Najua Mbowe amefanya mengi ila kama binadamu lazima amechoka na anahitaji usaidizi hivyo ameamua kujitokeza kumsaidia, niwashukuru wale wote walioniunga mkono licha ya masimango na matusi waliyoelekezewa," amesema Cecil Mwambe.
Mwambe amesema uchaguzi usio na ushindani hutoa viongozi ambao mwisho wa siku hudai kwanza sikutaka au nilishurutishwa.
Mbunge huyo amesema alianza kuona haja ya kugombea baada ya kumshuhudia Mbowe ambaye ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni akitishia kuachia nafasi hiyo kwa zaidi ya mara tatu.
Mwambe amesema anachotaka ni viongozi kuelewa kuwa uongozi ni dhamana ambayo mtu akiomba na kupewa ni lazima aithamini jambo ambalo yeye binafsi atafanya.
Amesema anaona mtazamo unaotolewa sasa kwa ngazi ya mikoa, wilaya na majimbo ni mdogo kulingana na umuhimu wa ngazi hizi na ndio maana amechukua fomu na tayari siku ya leo ameshairejesha makao makuu ya chama hicho, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Jana Jumatatu, baadhi ya vijana wa Chadema walijitokeza makao makuu ya chama hicho kumchukulia fomu Mbowe wakisema watakwenda kesho Jumatano kumshawishi ili agombee tena nafasi hiyo.