Zaidi ya asilimia 80 ya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, wamepatiwa chanjo ya Surua Rubella katika halmashauri ya Wilaya ya Singida kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi machi mwaka huu.
Mratibu wa Chanjo katika halmashauri hiyo Emmanuel Mawa anasema kuwa kwa kipindi hicho walilenga kuchanja watoto 2,648 lakini wakafanikiwa kuwapatia huduma hiyo watoto 2,345 sawa na asilimia 89, mbali na surua rubella, pia penta wametoa chanjo ya penta kwa watoto 2,571 sawa na asilimia 97 kwa lengo la kuwafikia watoto 2,648 na kuwapatia huduma hiyo ya chanjo bure. Hata hivyo amesema kuwa licha ya mafanikio hayo, lakini bado kuna changamoto ya baadhi ya wazazi na walezi kutojitokeza kuwapeleka watoto wao kwenye chanjo za aina mbalimbali, hali inayosababisha malengo yanayowekwa na halmashauri katika utoaji wa huduma hiyo kutofikiwa kwa asilimia 100.Wawa ametoa mwito kwa wazazi na walezi kuachana na imani potofu na kujenga utamaduni wa kuwapeleka watoto wao kwenye chanjo ili waweze kupata huduma hiyo kwani inatolewa bila malipo na ni salama na muhimu kwa ajili ya kuwakinga watoto dhidi ya magonjwa mbalimbali hatari.