Wananchi zaidi ya 40 wakiwemo madiwani kuandamana zaidi ya kilometa 120 hadi ofisi ya mkuu wa mkoa wa Geita june 3 kupinga njama za kutaka kupokonywa ardhi inayozalisha madini ya dhahabu katika machimbo ya Nyakafulu wilayani Mbogwe Mkoani Geita, ambapo tukio hilo limechukua sura mpya baada ya mkuu wa mkoa kutangaza kuunda kamati kuchunguza madai hayo.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel amesema ameamua kuunda kamati itakayovihusisha pia vyombo vya usalama kutokana na malalamiko ya walioandamana kuwatuhumu baadhi ya viongozi wa serikali kuu , halmashauri ya wilaya ya Mbogwe , chama cha mapinduzi na matajiri kuwa ndio walioko nyuma ya mgogoro huo ili kuwapokonya ardhi ambayo tayari ina uzalishaji wa madini ya dhahabu katika kijiji cha Nyakafulu. Mhandisi Robert Gabriel amesema kamati hiyo itachunguza na kuwahoji wote wanaotajwa kuwa nyuma ya mgogoro huo huku shauri lililotolewa uamuzi na Baraza la Ardhi na Nyumba la kata uliochangia kuibua maandamano hayo ameelekeza mdaiwa kukata rufaa katika Baraza la ardhi na nyumba la wilaya kwa hatua zaidi za kisheria.