Ushauri umetolewa kwa wanaume walioko katika wilaya ya Bunda mkoani Mara, kujenga tabia ya kuwasaidia wake zao, ambao ni wajawazito kwa kuwapeleka kliniki na kusikiliza ushauri wa wauguzi, badala ya kuwaacha wenyewe tu kwa kudhani kuwa jukumu hilo ni la mwanamke mwenyewe.
Ushauri huo umetolewa na baadhi ya wanaume waliojitokeza kwenye maadhimisho ya siku ya wauguzi duniani, yaliyofanyika katika viwanja vya kituo cha afya cha Bunda mjini kilichoko katika kata ya Kabarimu katika halmashauri ya mji wa Bunda. Aidha, baadhi ya wanawake wameizungumzia siku hiyo ya wauguzi duniani, huku wakiwaomba wauguzi kutekeleza wajibu wao ipasavyo, hasa wakati wakimuhudumia mama mjamzito. Baadhi ya wauguzi wamesema kuwa wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali pindi wanapopokea wagonjwa wakiwemo wajawazito, ikiwa ni pamoja na kutukanwa na baadhi ya watu. Katika maadhimisho hayo mkuu wa wilaya ya Bunda Lydia Bupilipili, amewataka wauuguzi wote wilayani hapo kutekeleza wajibu wao ipasavyo ikiwa ni pamoja na kujiamini.