Hali ya sintofahamu imezuka kwa wakazi wa kata ya Ruhembe wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro kufuatia watu 10 wakazi wa kata hiyo kupotea kwa siku 18 mara baada ya watu hao kudaiwa kwenda kufanya shughuli za kibinadamu katika hifadhi ya taifa ya Mikumi kinyume cha sheria na kupotelea huko mpaka sasa .
Tukio hilo la kupotea kwa watu hao 10 limetajwa kutokea Aprili mbili mwaka huu majira ya asubuhi mara baada ya watu hao kuaga kuwa wanakwenda shambani na kisha kuingia kwenye hifadhi ya taifa ya Mikumi kwa ajili ya kufanya shuguli mbalimbali za kibinadamu na baada ya hapo watu hao wakashindwa kurejea kijijini hatua iliyopelekea wananchi kuwa na mashaka na watu hao kutokana na siku kusonga mbele bila watu hao kurejeaa kijijini akibainishandiwani wa kata hiyo Salim Mponzi na mwenyekiti wa kijiji hicho Mohamed Kapyale.
Kufuatia tukio hilo imemlazimu kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro kamishna msaidizi mwandamizi wa jeshi la Polisi Wilbroad Mutafungwa kufika katika kijiji hicho na kuongea na wananchi kuhusu kutokea kwa tukio hilo huku akiwaomba wananchi hao kutoa ushirikiano kwa Jeshi la polisi ili kuweza kubaini mahali walipo watu hao .
Licha ya watu hao kupotea katika hifadhi ya Mikumi, watu wengine wanaoishi kijijini hapo wameendelea kufanya shughuli zao ndani ya hifadhi hiyo bila kuhofia chochote hatua inayomshangaza kamanda Mutafungwa huku uongozi wa kijiji ukiwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi.
Hata hivyo kamanda Mutafungwa amekemea tabia ya baadhi ya wananchi wanaopakana na hifadhi za taifa kufanya shughuli mbalimbali za kibinadamu ndani ya hifadhi hizo bila ya kuwa na kibali.
Jitihida za kuwatafuta watu hao bado zinaendelea kufanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na askari wa wanyama pori kutoka katika hifadhi ya Mikumi ili kujua kipi kimewapata watu hao.