Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, ameongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mikutano ya kipupwe(Spring Meetings) ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) inayofanyika mjini Washington DC, Marekani.
Akizungumza kwenye Ofisi za Ubalozi wa Tanzania Mjini Washigton DC, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amesema kuwa ujumbe wa Tanzania unaojumuisha pia wajumbe kutoka Serikali ya Mapinduzi-Zanzibar, utasimamia maslahi ya pande zote mbili za Muungano.
Mikutano hiyo inatoa fursa kwa Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu kutoka katika nchi wanachama ambao pia mi Magavana wa Benki ya Dunia na IMF, kujadili maendeleo na changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika utekelezaji wa masuala mbalimbali ya maendeleo na ushirikiano.
Aidha Mikutano hiyo hutoa fursa kwa nchi kushiriki kama mwanahisa kwenye mikutano ya kiutawala (Board of Governors) ya Taasisi hizo mbili ambapo maamuzi ya kiuendeshaji na kisera hufanyika
Tanzania itapata fursa ya kushiriki kwenye Kamati Maalum za Benki ya Dunia na IMF na baadhi ya mikutano hiyo ni Mkutano wa Mawaziri wa Fedha inayoshughulikia sera na utulivu wa Sekta ya fedha (International Monetary Committee and Finance Committee-IMFC
Dkt. Mpango atashiriki katika majadiliano na viongozi wa juu wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF wanaoshughulikia masuala ya Afrika kuhusu utekelezaji wa program za sera za kiuchumi, mikopo nafuu na misaada ya kitaalam kwa Tanzania