Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta John Magufuli amesema Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kufanikisha utafutaji na upatikanaji wa mafuta yaliyopo katika bonde la Eyasi Wembere na ziwa Tanganyika nchini ili Tanzania ianze kunufaika na rasilimali hiyo.
Rais Magufuli amesema hayo muda mfupi baada ya kupokea taarifa ya maendeleo ya utafiti wa mafuta katika maeneo ya bonde la ufa ya Eyasi Wembere na ziwa Tanganyika iliyowasilishwa na timu ya wataalamu wa Tanzania na Uganda.
Timu hiyo imeelezea uwepo wa viashiria vya uhakika vya kijiolojia vinavyothibitisha kuwepo kwa mafuta katika maeneo ya Senkenke, Mwanzugi na Kining’inila katika bonde la Manonga wilayani Igunga mkoani Tabora.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dokta Medard Kalemani na Balozi wa Uganda nchini Richard Kabonero, timu ya wataalamu hao imesema miamba, uoto na uwepo wa bonde Eyasi Wembere katika mfumo mmoja wa bonde la Afrika Mashariki unaofanana na maeneo mengine yaliyothibitika kuwa na mafuta ni kiashiria muhimu cha kuwepo mafuta.
Kutokana na taarifa hiyo, Rais Magufuli amewashukuru wataalamu wa Uganda wanaoshirikiana na wataalamu wa Tanzania katika kazi hii akiwaagiza wataalamu wa Tanzania kuendelea kufanya kazi kwa ukaribu na wataalamu wa Uganda ambao wana uzoefu wa kupata mafuta katika ziwa Albert nchini humo. Rais Magufuli amemuomba Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini wa Uganda Robert Kasande kumfikishia shukrani zake kwa Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni kwa ushirikiano anaoutoa kwa Tanzania katika kufanikisha upatikanaji wa mafuta nchini Tanzania.