Maafisa wa afya wa jiji la Wuhan lililokuwa kitovu cha mlipuko wa janga la virusi vya corona wametangaza kutokuwa na mgonjwa yoyote aliyelazwa hospitalini kutokana na maradhi yanayosambazwa na virusi hivyo.
Taarifa ya Wuhan kutokuwa na mgonjwa wa COVID_19 imetolewa na msemaji wa tume ya kitaifa ya afya nchini China, Mi Feng aliyezungumza na waandishi wa habari hii leo.
Taarifa hii ya karibuni zaidi inaonyesha hakuna maambukizi yoyote ya virusi vya corona kwenye jiji hilo, na imepongeza hatua za pamoja kati ya Wuhan na wahudumu wa afya kutoka maeneo mbalimbali nchini humo.
Jiji hilo liliripoti juu ya watu 46,452 waliougua homa ya mapafu COVID-19 sawa na asilimia 56 ya maambukizi yote nchini China, ambapo watu 3,869 walifariki dunia.