Rais wa Marekani Donald Trump ameweka saini kwenye sheria ya inayositisha visa kwa wahamiaji kuingia nchini humo kwa siku sitini.
Hayo yanajiri wakati mipaka ya Marekani ambayo imefungwa kufuatia kuzuka kwa ugonjwa hatari unaotikisa dunia wa Covid-19.
Katika taarifa iliyotolewa na Ikulu ya White House ilieleza kuwa "Rais Trump amesitisha visa kwa wahamiaji ili wafanyakazi na raia wa Marekani wawe wa kwanza kunufaika ndani ya taifa lao na uchumi kufunguliwa tena".
Marekani ni miongoni mwa nchi ambayo imeathirika zaidi duniani na ugonjwa wa Covid-19, ambao mpaka sasa vifo vya watu zaidi ya 45,000 vimeripotiwa kutokana na ugonjwa huo.
Hatua ya kubaki nyumbani, imetajwa kuwaathiri kiuchumi Wamarekani milioni 22 baada ya kukosa ajira katika wiki za hivi karibuni.
Sheria hii ya rais Trump inahusu Visa za kudumu na haiwagusi wafanyakazi katika sekta ya afya, kwakuwa wafanyakazi hao wanaonekana kuwa ni muhimu.
Aidha, sheria hiyo iliyowekwa saini na rais Trump haiwagusi watu ambao tayari wako nchini Marekani ambao wanatafuta kibali cha kuruhusiwa kupata ajira ndani.