Brussels:Viongozi wa Ulaya wanafanya kikao cha faragha leo kujadili kuhusu nyadhifa kuu za Umoja wa Ulaya, wakati mirengo pinzani katika bunge jipya la umoja huo ikijaribu kuunda mrengo wa siasa za wastani wenye viti vingi.
Uchaguzi wa mwezi uliopita barani Ulaya ulishuhudia vyama vinavyounga mkono sera za Umoja wa Ulaya na vya siasa za wastani za mrengo wa kushoto vikipambana kuhimili kishindo cha siasa kali za kizalendo, lakini hilo likawaacha viongozi wao wakiwa wametofautiana hata zaidi. Wadhifa unaogombaniwa ni wa mrithi wa Jean Claude Juncker kama Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya ambayo ndio taasisi yenye mamlaka makubwa ya Umoja wa Ulaya. Rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk anaongoza juhudi za viongozi hao kumtuewa mgombea kabla ya mkutano ujao wa kilele mnamo Juni 20 na 21, lakini dalili za mapema zinaonesha kuwa mazungumzo hayo yatakuwa marefu na magumu.
CHANZO: Idhaa ya Kiswahili DW