Leo ni Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, ambapo Umoja wa Mataifa umetumia siku hii kuwatunuku waandishi wawili wa shirika la habari la Reuters wanaotumikia kifungo cha miaka saba nchini Myanmar tuzo ya juu kabisa ya uhuru wa vyombo vya habari.
Wa Lone na Kyaw Soe Oo wametunukiwa tuzo katika mkesha wa maadhimisho ya siku hii, ambayo mwaka huu yanafanyika kimataifa nchini Ethiopia. Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) liliikabidhi Tuzo ya Uhuru wa Habari ya Guillermo Cano kwa Thura Aung, kaka yake Wa Lone, wakati wa sherehe hizo usiku wa kuamkia leo mjini Addis Ababa. Waandishi hao wawili walikamatwa mwishoni mwa mwaka 2017 wakati wakichunguza operesheni ya kijeshi na uvunjaji wa haki za binaadamu, yakiwemo mauaji ya kiholela, nchini Myanmar. Baadaye walitiwa hatiani kwa kuvunja Sheria ya Siri za Serikali. Umoja wa Mataifa na makundi mengine ya haki za binaadamu wamekuwa wakiishutumu serikali ya Myanmar kwa kuendesha kampeni ya kuwaangamiza Waislamu wa jamii ya Rohingya.
CHANZO: Idhaa ya Kiswahili DW