Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wanazingatia kutoa tamko la pamoja litakalohimiza kukomeshwa mara moja kwa mashambulizi ya kundi la Taliban nchini Afghanistan.
Rasimu ya tamko hilo iliyoshuhudiwa na shirika la habari la AP inaonya pia kwamba Baraza hilo halitaiunga mkono serikali yoyote itakayowekwa na nguvu za kijeshi ama kurudi kwa utawala wa Kiislamu wa Taliban uliokuwepo baina ya mwaka 1996 na 2001 nchini Afghanistan.
Tamko hilo ambalo ni la chini kuliko azimio, linatazamiwa pia kulaani mashambulizi ya Taliban dhidi ya miji mikubwa na midogo kote nchini Afghanistan.
Kwa mujibu wa nakala ya rasimu hiyo, Baraza la Usalama linaitaka serikali na kundi la Taliban kufanya mazungumzo yanayojumuisha makundi yote haraka iwezekanavyo na kufikia suluhisho la kisiasa la mgogoro wao.
Hayo yanajiri wakati Taliban ikiendelea kuchukuwa udhibiti wa majimbo, ambapo hadi sasa inahodhi majimbo 13 kati ya 34, likiwemo jimbo muhimu la Kandahar.