Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-Un amesema nchi yake inahitaji kujiandaa kwa mazungumzo na makabiliano na Marekani na haswa kujiandaa kikamilifu kwa mapambano.
Hii ni mara ya kwanza Bwana Kim kutoa maoni yake moja kwa moja juu ya utawala wa Rais Biden.
Korea Kaskazini ilikuwa imepuuza juhudi za serikali mpya ya Marekani kuanzisha mawasiliano ya kidiplomasia.
Bwana Kim alikuwa akizungumza kwenye mkutano wa viongozi wakuu huko Pyongyang.
Bwana Kim alisema wanahitaji kujiandaa kikamilifu kwa mapambano ili kulinda hadhi ya serikali yetu na masilahi yake kwa maendeleo huru, na vilevile kuhakikisha mazingira ya amani na usalama wa Korea Kaskazini, kulingana na chombo cha habari cha serikali KCNA.
Alisema pia Korea Kaskazini "kwa kasi na mara moja" itashughulikia maendeleo yoyote na "kuzingatia juhudi za kudhibiti hali kwa rasi ya Korea".
Maoni yake ya hivi karibuni yanakuja siku chache baada ya Bw. Kim kukiri rasmi kwamba Korea Kaskazini inakabiliwa na wasiwasi juu ya upungufu wa chakula.
Mnamo Aprili Bw. Biden aliitaja Korea Kaskazini kama tishio kubwa kwa usalama wa ulimwengu, na kusababisha jibu la hasira kutoka Korea Kaskazini ambayo ilisema taarifa hiyo ilidhihirisha dhamira ya Bwana Biden kuendelea kutekeleza sera ya uhasama kuelekea nchi hiyo.
Aidha, Washington pia hivi majuzi ilikamilisha ukaguzi wa sera yake ya Korea Kaskazini na kusema kuwa Marekani itaendelea kulenga hatimaye uharibifu kamili wa nyuklia katika peninsula ya Korea.