Somalia imetangaza kuwa inarejesha mahusiano ya kidiplomasia na nchi jirani ya Kenya baada ya kusitisha mahusiano hayo mwezi Desemba mwaka jana.
Mahusiano hayo ya kidiplomasia baina ya nchi hizo mbili yalikatishwa pale Somalia ilipoishutumu Kenya kuwa iliingilia siasa zao za ndani.
Naibu waziri wa habari wa Somalia Abdirahman Yusuf amesema sasa mahusiano ya kati ya nchi hizo mbili yamefufuliwa akiongeza Qatar ndiyo iliyoasaidia mchakato wa upatanisho.
Serikali ya Kenya haijatoa tamko kuhusiana na tangazo hilo la Somalia ila Ikulu ya Rais ya Nairobi iliandika katika ukurasa wa Twitter leo kuwa Rais Uhuru Kenyatta amekutana na Mfalme wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani na kupokea kile kilichotajwa ujumbe maalum.