Baraza la Seneti la Marekani limefikia uamuzi kuwa kesi dhidi ya rais wa zamani wa nchi hiyo Donald Trump sio kinyume cha katiba.
Mawakili wa Trump walikuwa wamepinga vikali mchakato huo, kwa hoja kuwa ilikuwa ukiukaji wa katiba kumfungulia mashtaka rais ambaye hayuko tena mamlakani, akiwa na hadhi ya raia wa kawaida.
Kwa upande mwingine, maseneta wa Chama cha Democratic walisema kwamba hata ikiwa rais ameondoka madarakani, anapaswa kuwajibishwa kwa matendo aliyoyafanya akiwa ofisini.
Kupitia kura iliyopigwa jana jioni, maseneta sita kutoka chama cha Republican cha Trump walijiunga na Wademocrat wote 50, na kupitisha uamuzi huo kwa kura 56 dhidi ya 44 zilizopinga.
Katika mashtaka hayo ambayo ni ya pili dhidi ya Trump, kiongozi huyo anatuhumiwa kuchochea uasi katika majengo ya bunge mjini Washington mnamo Januari 6 mwaka huu, ambamo watu watano walipoteza maisha.