Mahakama ya kijeshi ya Uganda imewahukumu kifungo cha siku 90 jela wanajeshi 7 baada ya kushtakiwa kwa kuwashambulia waandishi wa habari.
Jeshi la Uganda UPDF katika taarifa yake limesema kamati ya nidhamu ya jeshi imewahukumu wanajeshi hao akiwemo afisa wa cheo cha Kapteni, pamoja na kuwapa onyo kali.
Matukio ya kushambuliwa waandishi yameongezeka katika miezi ya hivi karibuni nchini Uganda, hasa wakati ambapo kumekuwa na operesheni za kuwakamata wafuasi wa kiongozi wa upinzani Bobi Wine.
Mnamo siku ya Jumatano wanajeshi walilivamia kundi la waandishi wa habari nje ya ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ambapo waliwapiga na 20 miongoni mwao walijeruhiwa.