Wizara ya Afya nchini Kenya imetoa taarifa ya nchi hiyo kukumbwa na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu ambapo mpaka sasa watu 13 wakiwemo watoto wenye umri chini ya miaka 10 wamefariki dunia kutokana na ugonjwa huo.
Waziri wa Afya Mutahi Kagwe amesema visa 550 vya ugonjwa huo vimeripotiwa mpaka sasa na tayari wataalam wa afya wamekwishaanza kuudhibiti ugonjwa huo.
Chanzo cha ugonjwa kinatajwa kuwa ni kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali.
Waziri Mutahi amesema anaamini inawezekana ugonjwa huo ukadhibitiwa ikizingatiwa kwamba umeripotiwa katika maeneo mawili pekee ndani ya nchi hiyo.