Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki, limepitisha azimio la kutaka kupitishwa kwa sheria ya kupiga marufuku utengenezaji na uingizwaji wa sabuni na vipodozi vyenye viambata vya sumu
vinavyodaiwa kuathiri afya za watumiaji hususani wanawake.
Hoja kuhusu katazo hilo imewasilishwa bungeni na Gideon Thoar, mbunge kutoka Sudan kusini, ambaye kwa kuzingatia vifungu kadhaa vya mkataba wa uanzishwaji wa jumuia ya Afrika Mashariki, kuhusu usalama wa bidhaa na kulinda afya ya mlaji, alitaka baraza la Mawaziri la jumuiya hiyo kukubali hoja na azimio la kupiga marufuku
uzalishaji, uingizwaji na matumizi ya sabuni na vipodozi vyenye Hydroquinone katika nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki.
Pamoja na kelele zinazopigwa na wana sayansi na magwiji wa tiba, vipodozi vyenye viambata vya sumu vinadaiwa kuendelea kuingizwa kwa wingi na kutumiwa katika nchi za Jumuiya ya Afrika mashariki. Mbunge Oda Gasinzigwa kutoka Rwanda, anasema hii ni ishara kuwa watumiaji wameukataa U-afrika wao.
Baadhi ya wabunge kutoka Burundi na Tanzania hususani wanawake, wanasema marufuku ya uingizaji na utumiaji wa vipodozi hivyo, itafanikiwa iwapo itakwenda sambamba na utoaji wa elimu kwa wananchi. Baada ya kupitishwa na bunge, hatua itakayofuata na kuwasilishwa kwenye mamlaka husika kwa hatua za kisheria.