Waziri wa elimu nchini Kenya George Magoha amewakumbusha walimu kwamba adhabu ya viboko imesalia kuwa marufuku katika shule za nchini humo.
Akiwa ziarani katika eneo la Pwani Magoha amesema walimu watakaopatikana wakiwapiga wanafunzi watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Kauli yake inajiri siku chache baada ya mwanafunzi katika eneo hilo kupigwa kwasababu ya kula chapati tano ikiwa ni zaidi ya zile ambazo walikuwa wamepangiwa kula.
Kipigo hicho kilimfanya mwanafunzi huyo wa kiume kupata majeraha kwenye figo na sehemu zake za siri na kulazwa hospitalini.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo na mwalimu mwingine walikamatwa na maafisa elimu mkoani humo walifunga shule hiyo baada ya ukaguzi kuonesha haijasajiliwa na ina masuala ya usafi.
Waziri Magoha amesema shule ambazo zina masuala ya kufuata sheria zitafungwa na wanafunzi kuchukuliwa katika shule za jirani.