Marekani imetoa taarifa ya kulaani vikali mapinduzi yaliyotokea Guinea, Ambapo imetoa taarifa hiyo imevitaka vyama vya siasa kuacha ghasia na kufuata sheria.
Marekani imesema kuwa ghasia na hatua zozote zile zilizopo nje ya katiba zitaathiri ustawi wa Guinea, amani na utulivu.
Aidha wamesisitiza kuwa midahalo ya kitaifa inapaswa kuwa ya wazi na inayolenga kupata suluhu ya demokrasia na amani.
Taarifa hiyo imekuja na taarifa nyingine za kimataifa kukemea kupinduliwa kwa rais Alpha Condé.
Jumuiya ya kiuchumi ya Afrika Magharibi, Ecowas, ililaani "jaribio la mapinduzi" na ikathibitisha "kutokubali mabadiliko yoyote ya kisiasa yanayopingana na katiba".
Imetaka rais Condé aheshimiwe na wale wote waliokamatwa pamoja naye waachiwe huru.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na Umoja wa Afrika tayari wameshutumu mapinduzi hayo na kutaka Rais Condé aachiwe huru.
Hatima ya rais huyo bado haijawekwa wazi baada ya video ambayo haijathibitishwa kuonesha Rais akiwa amezungukwa na askari ambao wanadai wamechukua mamlaka ya nchi.
Hata hivyo wizara ya usalama ilisema jaribio hilo la mapinduzi, liliweza kuzuiwa na walinzi wa rais.