Kundi la Taliban na serikali ya Afghanistan wanatarajia kuanza mazungumzo ya moja kwa moja ya amani Jumamosi, Septemba 12 huko Doha, nchini Qatar.
Mazungumzo hayo, yaliyocheleweshwa kwa zaidi ya miezi sita, yanatarajiwa kujaribu kumaliza karibu miaka 19 ya mgogoro kati ya pande hizo mbili hasimu nchini Afghanistan.
Chanzo cha serikali kimeliambia shirika la habari la AFP kuwa "Labda kujitokeze matatizo katika dakika za mwisho, timu ya (mazungumzo) ya serikali itaondoka kwenda Doha kesho, na tuna imani kuwa mazungumzo yatafanyika hivi karibuni, labda Jumamosi,".
Ikulu ya Rais nchini Afghanistan imeandika kwenye ukurasa wake wa Twitter, kwamba ujumbe wake wa watu 21 utaondoka kwenda Doha leo Ijumaa.
Kwa upande wa kundi la Taliban wametangaza kuwa wako tayari kushiriki mazungumzo hayo na wamesisitiza juu ya nia yao ya kuendeleza mchakato wa mazungumzo pamoja na kuleta amani kamili na mfumo safi wa Kiislam ndani ya mfumo wa maadili yao ya Kiislamu na masilahi yao ya kitaifa.