Zimbabwe imewazuia wafanyakazi wa umma ambao hawajanjwa kwenda kazini.
Waziri wa habari wa nchi hiyo Monica Mutsvangwa amesema kuwa serikali ilikuwa imewapatia wafanyakazi wake "muda wa kutosha " kupata chanjo za UVIKO-19.
Maafisa wanasema takriban 90% ya watu waliolazwa hospitalini wenye maradhi ya UVIKO-19 ni wale ambao hawakupokea chanjo.
Nchi hiyo ina wastani wa wagonjwa 145 wapya wa corona kila siku na imeripoti vifo saba Jumanne kutokana na ugonjwa huo.
Karibu Wazimbabwe milioni mbili, sawa na takriban 12% ya watu wa nchi hiyo kwa ujumla kwa sasa wamepata dozi kamili ya chanjo ya Corona.
Haifahamiki wazi ni wafanyakazi wangapi wa umma wameathiriwa na uamuzi huo wa baraza la mawaziri, na iwapo wataendelea kupokea mishahara au wataweza kufanya kazi nyumbani.
Serikali ni muajiri mkubwa zaidi, na agizo hilo linaweza kuathiri huduma kama vile za afya na elimu nchini humo, ambapo wengi wa waalimu wa shule za umma bado hawajapata chanjo ya corona.
Baada ya maambukizi ya Covid kupungua mwezi huu, kumbi za mazoezi ya mwili, migahawa na makanisa yaliruhusiwa kufungua milango, lakini wafanyakazi walikuwa bado hawajapata chanjo kamili.
Vyama vya wafanyakazi tayari vimeyapeleka makampuni mahakamani kwa madai ya ubaguzi dhidi ya wafanyakazi ambao hawajapokea chanjo.
#ChanzoBBCSwahili