Star Tv

Rais wa Zanzibar Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amezitaka taasisi zinazowasafirisha Mahujaji pamoja na Masheikh na Walimu kuendelea kuwapa moyo Waislamu waliokosa fursa ya kwenda Hijja kutokata tamaa.

Rais Dkt. Mwinyi aliyasema hayo leo Julai 21, huko katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Wete Pemba katika hotuba yake ya Baraza la Idd el Hajj aliyoitoa kwa wananchi.

Katika maelezo yake, Alhaj Dkt. Mwinyi alieleza kwamba wa wale ambao walifikia hatua ya kutoa gharama za safari waondolewe shaka kuwa fedha zao ziko salama hadi Mwenyezi Mungu atakapowezesha kwenda kutimiza wajibu huo kama walivyoazimia.

Aidha, Alhaj Dkt. Mwinyi alisema kuwa Serikali ya Saudia Arabia ilitangaza kuwazuia Waislamu kutoka nchi za kigeni kwenda kuitekeleza ibada ya Hijja kwa mwaka huu kutokana na kuendelea kuwepo kwa ugonjwa wa COVID-19 katika Mataifa mbalimbali duniani.

“Tulipokee tukio hili kuwa ni miongoni mwa mitihani ambayo Mwenyezi Mungu ametuahidi katika Kitabu chake Kitukufu cha Qurani kwamba atatutahini kwa namna mbali mbali. Hivyo”- Alisema Alhaj Dkt. Mwinyi.

Alhaj Dkt. Mwinyi alisema kuwa Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbali mbali kwa ajili ya kufanikisha dhamira ya kukifanya Kisiwa cha Pemba kuwa ni eneo maalum la kimkakati la uwekezaji.

“Tuendelee kuwa na subira na kushirikiana na Serikali ili kuweza kutimiza azma yetu hiyo” - alisema Alhaj Dkt. Mwinyi.

Katika kufikia dhamira ya kudumisha amani, Alhaj Dkt. Mwinyi aliwahimiza wananchi wote kuungana katika mapambano dhidi ya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia na watoto pamoja na biashara haramu na matumizi ya dawa za kulevya.

“Tuwaase watoto wetu wajiepushe na marafiki wabaya, waongeze bidii na waweke mazingatio zaidi katika masomo yao ili tupate raia wema, wazalendo,wenye taalumu na maadili mema”- Alisisistiza Alhaj Dkt. Mwinyi.

Mapema asubuhi, Alhaj Dkt. Mwinyi aliungana pamoja na Waumini wa Dini ya Kiislamu katika ibada tukufu ya swala ya Eid-el Hajj iliyoswaliwa katika viwanja vya Mnazi Mmoja Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Waislamu mbalimbali wamehudhuria katika viwanja hivyo na kuungana pamoja na Rais Dkt. Mwinyi katika kutekeleza Ibada ya Swala ya Eid ya kuchinja ambayo huswaliwa baada ya waumini kutekeleza ibada tukufu ya Hijja huko Makka.

Viongozi kadhaa waliohudhuria katika hafla hiyo akiwemo Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Masoud Othman, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdullah, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabih, Mawaziri, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Al Maulid, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, wake wa viongozi wa kitaifa wakiongozwa na Mama Mariam Mwinyi pamoja na viongozi wanawake pamoja.

Latest News

Mgogoro wa Maji unatishia Amani Duniani, inasema ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa...
21 Mar 2024 14:18 - Kisali Shombe

Siku ya Maji Duniani ambayo inafanyika tarehe 22 Machi ikiwa na kaulimbiu: 'Maji kwa Ustawi na Amani. Ambapo maji ni moj [ ... ]

Matarajio katika mkutano wa BRICS nchini Afrika Kusini, Jumanne tarehe 22/2023
21 Aug 2023 12:14 - Kisali Shombe

Mkutano huo ambao utafanyikia Johannesburg nchini Afrika Kusini siku ya Jumanne, tarehe 22 Agosti 2023, unatarajiwa kuhu [ ... ]

Rais Ramaphosa Kuwa Mwenyeji wa Rais Xi Jinping wa China
21 Aug 2023 11:11 - Kisali Shombe

Rais Cyril Ramaphosa Jumanne ya tarehe 22 Agosti 2023, atakuwa mwenyeji wa Mheshimiwa Rais Xi Jinping wa China katika Zi [ ... ]

Other Articles

Social Media

Copyright © 2024 . Star Tv - Tanzania. All Rights Reserved.