Star Tv

Zaidi ya wanajeshi 1,000 wa Afghanistan wamekimbilia nchi jirani ya Tajikistan baada ya kukabiliana na wanamgambo wa Taliban.

Wanajeshi walikimbilia mpaka wa nchi hiyo jirani ili kuokoa maisha yao wenyewe, kulingana na taarifa ya walinzi wa mpaka wa Tajikistan.

Vurugu zimeongezeka nchini Afghanistan, na Taliban wamekuwa wakifanya mashambulizi na kuchukua maeneo zaidi katika wiki za hivi karibuni.

Idadi kubwa ya vikosi vya kigeni vilivyobaki nchini Afghanistan vimeondolewa kabla ya tarehe ya mwisho ya Septemba, na kuna wasiwasi kwamba jeshi la Afghanistan litaporomoka.

Chini ya makubaliano na Taliban, Marekani na washirika wake wa NATO walikubaliana kuondoa wanajeshi wote kwa ahadi ya wanamgambo kutoruhusu Al-Qaeda au kikundi kingine chochote chenye msimamo mkali kuhudumu katika maeneo wanayodhibiti.

Kamati ya Usalama ya Kitaifa ya Tajikistan, ambayo inasimamia usalama wa mpaka, ilisema kwamba wanajeshi wa Afghanistan walitafuta hifadhi mapema Jumatatu asubuhi baada ya kupigana na wanamgambo wakati wa usiku, kulingana na shirika la habari la serikali la Tajikstan, Khovar.

"Walinzi wa mpaka wa Tajik kwa sasa wanadhibiti hali katika mpaka wa Tajikistan na Afghanistan,"- ilisema Kamati ya Usalama.

Taliban sasa inadhibiti karibu theluthi moja ya Afghanistan, na inaendelea kukamata maeneo zaidi kila siku.

Mikoa ya Badakhshan na Takhar, ambayo inapakana na Tajikistan, imeshuhudia harakati za hivi karibuni za Taliban kuteka maeneo makubwa

Hii ni mara ya tatu kwa wanajeshi wa Afghanistan kukimbilia Tajikistan katika siku tatu zilizopita na kisa cha tano katika wiki mbili zilizopita. Imefikisha jumla ya wanajeshi waliorejea Tajikistan kufika takriban 1,600.

Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani anasisitiza kuwa vikosi vya usalama vya nchi hiyo vina uwezo kamili kuwazuia waasi, hata hivyo kumekuwa na ripoti za wanajeshi zaidi wanaotafuta hifadhi nchini Pakistan na Uzbekistan kutoroka vita.

Nchi za jirani, pamoja na zile za Asia ya Kati, zinajiandaa kwa wakimbizi ikiwa vita vitaendelea nchini Afghanistan.

Lyse Doucet, mwandishi mkuu wa BBC wa kimataifa, amesema hali ya hofu na kutojua hatima ya maisha yao inatawala watu wengi nchini Afghanistan.

"Hawana uhakika kuhusu nchi yao inaelekea wapi, hawana uhakika kuhusu kijiji chao au mji au jiji, na hawana uhakika juu ya maisha yao wenyewe na hatima ya familia zao,"- alisema.

Hata hivyo msemaji wa Taliban Suhail Shaheen aliambia BBC kuwa Taliban hawahusiki na ongezeko la vurugu hivi karibuni.

 

Latest News

RAIS WA UKRAINE AAMURU RAIA WOTE KUHAMA MKOA WA DONETSK.
31 Jul 2022 17:17 - Grace Melleor

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameamuru raia wote ambao bado wanaishi katika maeneo ya mashariki mwa mkoa wa Donetsk [ ... ]

KIFO CHA RAIA WA NIGERIA NCHINI ITALIA CHAZUA HASIRA.
31 Jul 2022 16:58 - Grace Melleor

Kifo cha mhamiaji aliyeshambuliwa mchana kweupe nchini Italia kimezua hasira.

VUTA N’KUVUTE YA MANARA NA KATIBU WA TFF YAIBUKA.
25 Jul 2022 16:37 - Grace Melleor

Katibu Mkuu wa Shrikishi la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Kidao Wilfred amesema amesekitishwa na madai ya yaliyekuwa Af [ ... ]

Other Articles

Social Media

Copyright © 2022 . Star Tv - Tanzania. All Rights Reserved.