Mamlaka ya mapato nchini Kenya (KRA) inatarajiwa kuzifungia jumla ya nambari ya siri 66,269 za kulipa kodi ambazo hazitumiki kufikia Alhamisi wiki hii, ripoti za vyombo vya habari nchi humo zimesema.
Wamiliki wa nambari hizo za siri za kulipa kodi ambao ni pamoja na watu binafsi na mashirika ya biashara huenda wakafutiwa usajili malipo ya ushuru wa bidhaa.
Walipa kodi watakaoathiriwa watazuiwa kutoza ada ya ushuru wa bidhaa katika biashara zao na huenda wakakabiliwa na vikwazo vingine vya utozaji ushuru.
Hatua kama hiyo pia itachukuliwa dhidi ya watu ambao hawajakuwa wakijaza fomu ya kuthibitisha wanalipa kodi kwa mujibu wa sheria.
“Kufutiwa kwa jukumu la kulipa ushuru wa bidhaa ni mpango unaoendelea, utawaathiri walipa kodi ambao hawatajaza fomu ya kila mwezi ya kuthibitisha wamelipa ushuru wa bidhaa au wale ambao hawaoneshi jinsi walivyolipa ushuru huo kila mwezi miongoni mwa mambo mengine,”-KRA ilisema katika taarifa yake kwa umma.