Wizara ya mambo ya ndani ya Iraq imesema watu 82 wamekufa huku wengine 110 wakijeruhiwa katika mkasa mkubwa wa moto katika vyumba vya wagonjwa mahututi katika hospitali moja mjini Baghdad inayowahudumia wagonjwa wa virusi vya corona.
Mamlaka ya hospitali hiyo imelaumiwa kwa uzembe kufuatia moto huo unaosemekana ulitokea baada ya mitungi ya gesi ya hewa ya Oksijeni kuripuka katika hospitali ya Ibn al Khatib.
Waziri Mkuu wa Iraq Mustafa al-Kadhimi aliwafuta kazi maafisa kadhaa wa hospitali hiyo saa chache baada ya mkasa wa moto.
Wizara ya afya nchini humo imesema watu 200 waliokolewa lakini hadi sasa bado baadhi ya jamaa za wagonjwa wangali wanaitafuta miili ya wapendwa wao.