Star Tv

Familia ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere imefika wilayani Chato Mkoani Geita nyumbani kwa Mjane Mama Janeth Magufuli kumpa salamu za pole kutokana na msiba wa aliyekuwa mumewe Hayati Rais Dkt. John Magufuli.

Akizungumza kwa niaba ya familia ya Baba wa Taifa, Msemaji wa familia ya Mwalimu Nyerere kutoka Ukoo wa Burito, Chifu Japhet Wanzangi amesema wamefika kutoa salamu za rambirambi kwa Mama Janeth Magufuli kutokana na kuguswa na msiba huo.

Chifu Wanzagi amesema salamu hizo za rambirambi walizotoa zimeambatana na ng'ombe dume mmoja kama sehemu ya kumtia faraja Mjane wa Marehemu kulingana na mila na desturi za kabila la Wazanaki.

"Tumekuja kuwakilisha salamu za ukoo, tunashukuru kwamba baada ya mazishi, tumeweza kupata nafasi ya kufika nyumbani kuonana na Mjane Mama Janeth na familia, tumekuja kuhani na tumetoa ng'ombe mmoja dume kama rambirambi yetu"- Msemaji wa familia ya Mwalimu Nyerere Chifu Japhet Wanzangi.

Aidha, Chifu Wanzangi amewasilisha salamu za pole kwa Mama Janeth Magufuli zilizotumwa na Mama Maria Nyerere ambaye amemtakia heri na nguvu ya ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu anachopitia.

"Hayati Dkt. Magufuli tutamkumbuka kwa mengi, amefanya kazi nzuri na kubwa katika taifa. Neno la Mungu linasema, kuwakumbuka wenye haki ni baraka, kitabu cha Methali sura ya 10 mstari wa 7 maandiko yanasema, kuwakumbuka wenye haki ni baraka bali jina la mtu mwovu litaoza"- alisema Wanzagi.

Kwa upande wake mama Janeth Magufuli amepokea salamu hizo za rambirambi, ambapo amesema amefarijika kutokana na salamu hizo zilizotolewa na Mama Maria Nyerere.

"Msalimieni sana Mama Maria Nyerere, mfikishieni salamu, mwambieni nampenda, ni mama yangu, tuko pamoja na asante kwa zawadi nzuri aliyonipa, ameniheshimisha Mama huyu na alikuwa na upendo kwenye familia yangu na Mume wangu pia, Mungu ambariki sana na nyie mliokuja Mungu awabariki"-Mke wa Hayati Rais Dkt. John Magufuli Mama Janeth Magufuli.

Hayati Rais Dkt. John Pombe Magufuli alifariki Dunia Machi 17, katika hospitali ya Mzena Jijini Dar es Salaam kutokana na Maradhi ya moyo na amezikwa Machi 26, 2021.

Latest News

Mgogoro wa Maji unatishia Amani Duniani, inasema ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa...
21 Mar 2024 14:18 - Kisali Shombe

Siku ya Maji Duniani ambayo inafanyika tarehe 22 Machi ikiwa na kaulimbiu: 'Maji kwa Ustawi na Amani. Ambapo maji ni moj [ ... ]

Matarajio katika mkutano wa BRICS nchini Afrika Kusini, Jumanne tarehe 22/2023
21 Aug 2023 12:14 - Kisali Shombe

Mkutano huo ambao utafanyikia Johannesburg nchini Afrika Kusini siku ya Jumanne, tarehe 22 Agosti 2023, unatarajiwa kuhu [ ... ]

Rais Ramaphosa Kuwa Mwenyeji wa Rais Xi Jinping wa China
21 Aug 2023 11:11 - Kisali Shombe

Rais Cyril Ramaphosa Jumanne ya tarehe 22 Agosti 2023, atakuwa mwenyeji wa Mheshimiwa Rais Xi Jinping wa China katika Zi [ ... ]

Other Articles

Social Media

Copyright © 2024 . Star Tv - Tanzania. All Rights Reserved.