Hospital ya Rufaa ya KCMC iliyopo Moshi Mkoani Kilimanjaro imeanza kuzalisha hewa ya oksijeni kama moja ya harakati za kukabiliana na upungufu hewa hiyo inayotumika kwa wagonjwa wenye mfumo hafifu wa upumuaji ikiwa pamoja na Watoto njiti.
Taarifa zaidi na Zephania Renatus…………
Inaelezwa kuwa teknolojia ya matumizi ya hewa ya Oksijeni katika taasisi za afya mahala popote ulimwenguni ni moja ya tiba muhimu hususani kwa wagonjwa wenye mfumo hafifu wa upumuaji.
Watoto waliozaliwa chini ya umri nao wanaelezwa kuwa wanatumia hewa ya Oksijeni kama moja ya tiba yao ya kuwawezesha kupumua kwa urahisi.
Hospitali ya Rufaa ya KCMC iliyopo Mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro imeazimia kumaliza tatizo la Uhaba wa hewa ya oksijeni katika hospitali zilizopo ukanda wa kaskazini baada ya kukamilisha ujenzi wa kinu cha kuzalisha hewa hiyo.
Mhandisi wa Kinu cha kuzalisha hewa hiyo katika Hospitali ya KCMC Danstan Kanza,amesema kinu hicho kina uwezo wa kuzalisha hadi mitungi mia nne kwa siku ,na uzalishaji huo umeanza January 13 mwaka huu.
Madaktari katika wodi ya Watoto waliozaliwa chini ya umri wamesema hewa ya Oksijeni ni moja ya tiba muhimu katika kuwawezesha watoto hao kuendelea kuishi.
Kukamilika kwa Kinu hicho sasa kunatarajiwa kumaliza changamoto ya uhaba wa Hewa ya Oksijeni kwa hospitali zilizopo ukanda wa Kaskazini hususani mikoa ya Kilimanjaro,Arusha na Manyara ambapo itasaidia kutatua tatizo la upumuaji kwa wagonjwa na watoto wanaozaliwa kabla muda wao (watoto njiti).
Mwisho.