Vifaa vilivyokuwa vikitumiwa na mamlaka ya vitambulisho vya taifa NIDA katika kuandikisha vitambulisho vya taifa kwenye halmshauri ya wilaya ya Arusha iliyopo mkoani Arusha ,vimeibiwa na watu wasiojulikana.
Mkuu wa wilaya ya Arumeru Jerry Muro ametoa siku tatu kwa watu waliohusika na wizi huo kuvirejesha vifaa hivyo kwa hiyari mara moja kabla ya msako msako mkali kupitia vyombo vya dola kuanza.
Muro ametoa kauli hio katika ofisi hizo za halmashauri ya Arusha ambapo amesema baada ya siku tatu kupita watu walioiba vifaa hivyo wasiporejesha hatua kali itatolewa kwa yeyote atakae kutwa na kifaa chochote ambacho ni mali ya serikali.
“Namimi niseme siko tayari kuona wilaya inahujumiwa, vitu vilivyoko kwenye wilaya vinahujumiwa alafu nikakaa kimya, niwaombe wananchi mtupatie ushirikiano lakini kwa wale waliohusika tunatoa siku tatu za kujisalimisha endapo vifaa havitarudishwa kwa hiyari tutachukua hatua.”-Jerry Muro-Mkuu wa wilaya ya Arumeru.
Muro amesema vifaa vilivyoibwa ni kamera mbili, stendi mbili, kompyuta mpakato mbili, kompyuta moja aina ya Desktop, stendi mbili, Extension mbili, pamoja na keyboad.
Amewaomba wananchi kutoa taarifa pindi watakapoona mtu yeyote anauza vifaa hivyo vilivyoibiwa na kuwataka wasinunue kamera ,kompyuta ama vitu vilivyoibwa na kuwataka wananchi hao kutoa taarifa pindi watakapona mtu yeyote anauza vifaa hivyo .
Aidha,mesema kuibiwa kwa vifaa hivyo si mara ya kwanza kutokea kwenye ofisi za NIDA za Arumeru na upelelezi wakubaini juu ya wizi wa vifaa hivyo unaendelea.
Baadhi ya wafanyakazi katika ofisi hiyo wameeleza hali waliyokumbana nayo baada ya kufika ofisini na kulazimika kutoa taarifa kwa mamlaka husika.
Wilson Boaz ambaye ni mfanyakazi wa halmashauri ya wilaya ya Arumeru amesema alibaini wizi wa vifaa hivyo mara tu alipofika ofisini hapo.
“nilipofungua nilikuta mlango uko wazi ndipo nilitoa taarifa kwa mlinzi aliyekuwa zamu”-Wilson Boaz, Mfanyakazi wa halmashauri wilaya ya Arumeru.
Kamanda wa polisi mkoa Arusha Jonathan Shana amethibitisha kuripotiwa tukio hilo na amesema upelelezi umeshaanza na pindi utakapokamilika taarifa rasmi ya polisi itatolewa.
Mwisho.