Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi Wakurugenzi saba wa Tume ya Umwagiliaji akiwemo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa tume hiyo ili kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zinazowakabili.
“CAG afanye haraka uchunguzi wa kina, tunataka kujua ni nani alikuwa mlango wa ubadhirifu huu. Hatutamuonea mtu, wote watakaothibitika kuhusika na matumizi mabaya ya fedha watachukuliwa hatua.” Waziri Mkuu amechukua hatua hiyo wakati wa kikao na viongozi wa tume hiyo kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Hazina, jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Mawaziri, Manaibu Waziri na Makatibu Wakuu. Mbali na kuwasimamisha kazi wakurugenzi hao, pia Waziri Mkuu ameagiza watumishi wengine 21 wa tume hiyo wachukuliwe hatua za kinidhamu kutokana na utendaji usioridhisha kwenye miradi mbalimbali inayosimamiwa na tume hiyo. Waziri Mkuu amesema Serikali imechukua hatua hiyo kutokana na udhaifu wa kiutendaji ndani ya tume hiyo ikiwemo matumizi mabaya ya fedha za miradi, rushwa, matumizi mabaya ya madaraka, upendeleo na kukosa umakini. “Hatua kali zitachukuliwa dhidi ya ubadhirifu uliofanyika katika miradi ya umwagiliaji.” Amesema hali ya kilimo cha umwagiliaji nchini hairidhishi na Serikali haijafurahishwa na utendaji wa Tume ya Umwagiliaji licha ya kuwekeza nguvu kubwa, hivyo inataka kuona mabadiliko.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa amesema miradi mingi ya umwagiliaji ilifeli kwa sababu ya ilijengwa chini ya kiwango hususani mabwawa na pia haikuwa ikilingana na kiasi cha fedha kilichokuwa kinatolewa. “Mradi wa kutumia sh. bilioni mbili wanatumia sh. bilioni nne.”
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu, Dodoma.