Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kuendeleza zao la zabibu ili kuhakikisha linaleta tija kwa wakulima.
Waziri Mkuu amebainisha hayo wakati alipotembelea Kituo cha Utafiti wa Kilimo Tanzania katika eneo la uzalishaji miche ya zabibu, mashamba na viwanda vya zabibu, Dodoma.
“Serikali imeanzisha kampeni ya kuhamasisha kilimo cha zao la zabibu, tunataka kumsaidia mkulima kuanzia maandalizi ya shamba, upatikanaji wa pembejeo hadi hatua ya mauzo.”
Waziri Majaliwa ametembelea kituo hicho cha utafiti kuona uwezo wake wa kuzalisha mbegu, pia ametembelea mashamba ya wakulima katika eneo la Msalato na Hombolo ili kuhamasisha kilimo hicho.
Pia, Waziri Mkuu ametembelea kiwanda vya kuchakata zabibu kikiwemo kiwanda kidogo cha mkulima mdogo wa zabibu Bw. Phortunatus Kenyunko kilichopo eneo la Msalato, jijini Dodoma.
Mbali na kutembelea kiwanda hicho kidogo, pia Waziri Mkuu ametembelea kiwanda kikubwa cha kutengeneza mvinyo wa zabibu cha Cetawico kiilichopo Homboro, jijini Dodoma.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wakulima wa zabibu kwamba Serikali imedhamiria kuboresha kilimo cha zao hilo kwa sababu kilimo ni mkombozi kwa Watanzania.
Amesema kampeni hiyo itanzia mkoa wa Dodoma kwa kuwa imegundua kwamba zabibu ni fursa ya kiuchumi nchini na ardhi yote ya wilaya za mkoa wa Dodoma inakubali kilimo hicho.
Katika kuhakikisha kilimo hicho kinapata mafanikio, Waziri Mkuu amezitaka taasisi za kifedha ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ibadilike na kutoa mikopo kwa wakati.