Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli anasikitika kutangaza kifo cha Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi Dkt.Augustine Mahiga (Mbunge) kilichotokea leo Alfajiri tarehe 01 Mei,2020. Jijini Dodoma.
Mhe.Balozi Mahiga ameugua akiwa nyumbani kwake Jijini Dodoma na amefikishwa hospitali akiwa ameshafariki dunia.
Rais Magufuli ametoa salamu zake za pole kwa familia ya Marehemu, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai, Wabunge, Wafanyakazi wa Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na wananchi wa Iringa, ambapo amesema anaungana nao katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.
Aidha, amemuelezea Marehemu Balozi Mahiga kama mchapakazi, muadilifu, mzalendo na mwanadiplomasia mahiri aliyeiwakilisha na kuipigania Tanzania katika Nyanja za Kimataifa kwa miaka mingi.