Viongozi mkoani Tabora wameiomba serikali kuhakikisha inawakamata watu waliohusika katika tukio la mauaji ya Diwani wa Kata ya Usunga Alfed Masamalo wilayani Sikonge mkoani Tabora.
Taarifa na Sunday Kabaye
Viongozi hao wakiwemo wa dini wametoa ombi hilo kwa serikali kufuatia kutokea kwa matukio ya mauaji mfululizo ikiwemo tukio la kukatwakatwa mapanga kwa Mhandisi wa maji katika wilaya ya Sikonge hadi umauti kumpata siku za hivi karibu.
Baada ya kupokea maombi kutoka kwa viongozi hao Mkuu wa mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri ambaye aliongoza mamia ya wakazi wa mkoa wa Tabora katika mazishi ya diwani huyo aliyeuwawa kwa kukatwa mapanga katika sehemu za mwili wake ameagiza vyombo vya usalama kuhakikisha wanafanya operesheni na kuwakamata wote wanaohusika na matukio ya mauaji yanayoendelea mkoani Tabora
Kwa upande wake Kaimu Kamanda wa polisi mkoa wa Tabora Kamishina Msaidizi wa Polisi Laurian Fabian amesema tayari jeshi hilo linawashikilia watu sita wanaotuhumiwa kuhusika na tukio la kifo cha diwani huyo.
Katika maeneo mbalimbali ya mkoani Tabora hivi karibuni kumekuwepo na mfululizo wa matukio ya watu kuuawa kikatili wakiwemo Wananchi na watumishi wa serikali jambo linaloanza kuleta hofu kwa wakazi wa mkoa wa Tabora.
Mwisho.