Star Tv

Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amewasimamisha kazi wahandisi wote wa Maji Wilaya ya Busega RUWASSA wanaosimamia mradi wa maji Lamadi na kuagiza wapangiwe kazi nyingine, huku akiwaweka ndani watu wanne, wakiwemo wahandisi wawili washauri wa mradi, kutokana na kushindwa kutimiza majukumu yao ipasavyo katika usimamizi wa mradi wa maji Lamadi unaojengwa na serikali kwa gharama ya shilingi bilioni 12.8.

Tatizo limeanzia kwenye  mkutano uliokuwepo baina ya wananchi na naibu waziri wa maji ambapo wananchi wa Lamadi waliweka mambo hadharani kubainisha changamoto zilizopo katika mradi huu wa maji.

Ndipo ikawa mguu kwa mguu kuangalia dosari zilizopo, ambapo Naibu Waziri Maji Jumaa Aweso, na  akabaini hujuma kadhaa katika utekelezaji wa mradi huo licha ya mabomba kuwekwa chini ya kiwango, lakini  jambo la mwekezaji wa kampuni ya ASHICO kuwekewa maji lilibainika ni lenye utata.

Baada ya kujionea changamoto za mradi huo Naibu Waziri Aweso akaagiza watu waliozembea katika utekelezaji wa mradi huu kuwekwa ndani, wakiwemo wahandisi washauri wawili wa mradi

Naibu waziri ametoa maelekezo ya serikali kwa mkandarasi wa kampuni ya kichina ya China Civil Engineering Construction Cooperation, anayejenga kwa gharama ya sh. bilioni 12.8, kurekebisha dosari za mradi huo kwa gharama zake.

Awali Mbunge wa Busega, Dkt. Raphael Chegeni, alimweleza Naibu Waziri kilio cha wananchi wa Lamadi ni kupata maji safi na salama, hivyo ni vyema changamoto zinazokwamisha zikatatulia haraka.

Makabidhiano ya awali ya mradi huo yamefanyika novemba, 22, 2019, ambapo  mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira jijini Mwanza (Mwauwassa) ndio wasimamizi wa mradi huo.

               MWISHO

 

Copyright © 2020 . Star Tv - Tanzania. All Rights Reserved.