Waziri wa mambo ya ndani ya nchi Kangi Lugola amemtaka kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Hamis Issa kurudi mkoa wa Kilimanjaro na kuhakikisha mwananchi Hemed Mbaga aliyebambikizwa kesi anatolewa mahabusu.
Waziri Lugola ametoa agizo hilo jijini Dodoma katika ufunguzi wa bonanza la michezo kati ya madereva wa bodaboda, bajaji na askari polisi. Waziri Lugola amemtaka Kamanda wa Polisi Hamis Issa ambaye amehamishiwa mkoani Morogoro ahakikishe anarejea mkoani Kilimanjaro kufikia kesho ili kushughulikia kesi hiyo ya kubambikizwa kwa Bw. Mmbaga na kumtoa mahabusu. Aidha waziri lugola amekemea tabia ya baadhi ya askari polisi wasio waadilifu kuwabambikiza kesi wananchi, huku akimuagiza kamanda wa polisi wilaya ya Dodoma kuorodhesha idadi ya madereva wa bodaboda na bajaji waliobambikizwa kesi katika wilaya hiyo. Baadhi ya wananchi wakiongozwa na mbunge wa jimbo la Dodoma mjini Anthony Mavunde wakaeleza namna ambavyo polisi wamekuwa wakiwabambikiza kesi wakiwemo madereva bajaji na bodaboda wanapokuwa vijiweni.