Star Tv

Licha ya wanawake kuwa mstari wa mbele katika kudai haki sawa na kupinga ukatili unaofanywa dhidi yao na baadhi ya wanaume, imebainika kuwa wanawake wamekuwa wakiongoza kwa kufanya ukatili majumbani hasa kwa watoto.

Mratibu wa Jukwaa la Mwanamke Jitambue Mwinjilisti Nuruted Mkami katika uzinduzi wa jukwaa hilo wilayani Tarime mkoani Mara amewataka wanawake kuacha ukatili huo ambao kwa kiasi kikubwa unasababisha wafanyiwe ukatili.

Wanawake ndio kundi kubwa ambalo limekuwa lilalamika kufanyiwa ukatili ikilinganishwa na wanaume, lakini Mratibu wa Jukwaa la Mwanamke Jitambue, Mwinjilisti Nuruted Mkami, amesema ukatili na unyanyasaji wa kijinsia wanaofanyiwa wanawake majumbani mara nyingi wamekuwa wakiusababisha wenyewe kwa kuwa makatili hasa dhidi ya watoto, hivyo wanapodai usawa katika jamii ni lazima wajitambue kwa kuacha ukatili huo na kujishughulisha zaidi na shughuli za uzalishaji mali.

Jukwaa la Mwanamke Jitambue limeanzishwa kutokana na wanawake wengi kutojitambua, ambapo maono ya kuanzishwa kwake ni Tarime, na shabaha yake kubwa ni kutoa elimu na kuwasaidia wanawake wanaofanyiwa ukatili wa aina mbalimbali.

Mgeni Rasmi katika uzinduzi wa Jukwaa hilo, Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Wilaya ya Rorya, Samweli Kiboye (No.3), amewataka kina mama kujitambua na kumtanguliza Mungu katika kila jambo wanalofanya, huku akiwataka wanaume kuwapa fursa wanawake kushiriki kikamilifu katika shuguli za uzalishaji mali.

Copyright © 2020 . Star Tv - Tanzania. All Rights Reserved.