Star Tv

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa ameuagiza uongozi wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), kutengeneza mifumo ya kielektroniki itakayomuwezesha mtu yeyote anayehitaji huduma ya mkalimani wa lugha na hasa lugha ya Kiswahili, kuipata huduma hiyo kwa njia ya mtandao na kwa haraka zaidi.

Waziri Bashungwa ametoa agizo hilo leo Agosti 21, 2021 wakati akizindua vifaa vya kuwezesha ukalimani, katika hafla fupi ya uzinduzi iliyofanyika ofisi za Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) jijini Dar es Salaam.

Waziri Bashungwa amesema, Serikali kupitia kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu, imetoa kiasi cha zaidi ya shilingi Milioni 187 kugharamia ununuzi wa vifaa hivyo, ikitarajia kuona mabadiliko chanya ya taaluma hiyo kwa manufaa ya wengi wenye uhitaji na kwa ajili ya uendelezaji wa lugha ya Kiswahili kitaifa na kimataifa.

“Ili kuenenda sawa na uwekezaji huu, nawaagiza BAKITA wekezeni nguvu kwenye kubuni mifumo ya kielekroniki itakayomuwezesha mtu kuomba na kupatiwa mkalimani kwa njia ya mtandao, hatuwezi kwenda kizamani zamani lazima twende kidigitali ndiyo maana halisi ya uwekezaji huu.” -alisema Waziri Bashungwa.

Aidha Waziri Bashungwa amesema watanzania wote wanawajibika kuiendeleza zaidi lugha ya Kiswahili kwa kuwa Tanzania ndiyo chimbuko la lugha hiyo.Hivyo kama taifa, lina wajibu wa kuhakikisha wanaohitaji kujua kiswahili wanapatiwa rasilimali mbalimbali zitakazo wawezesha kukielewa na kukitumia kwa usanifu na ufasaha zaidi.

Awali akizungumza katika hafla hiyo Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul amesisitiza matumizi na utunzaji mzuri wa vifaa hivyo ili kutimiza azima ya Serikali ya kuendeleza utaalamu wa ukalimani nchini.

Kwa upande wake kaimu katibu mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) Bi. Consolata Mushi, amesema vifaa hivyo vilivyonunuliwa vina uwezo wa kuwezesha jumla ya lugha nane kufanyiwa ukalimani kwa wakati mmoja.

Vifaa hivyo vinajumuisha chombo maalumu kwa ajili ya kuchagua lugha na kuzungumza, seva, vipaza sauti, visikizi, spika, kikuza sauti na mashine ya mkalimani, ambavyo vinaweza kutumiwa na watu thelathini kwa wakati mmoja.

Latest News

Mgogoro wa Maji unatishia Amani Duniani, inasema ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa...
21 Mar 2024 14:18 - Kisali Shombe

Siku ya Maji Duniani ambayo inafanyika tarehe 22 Machi ikiwa na kaulimbiu: 'Maji kwa Ustawi na Amani. Ambapo maji ni moj [ ... ]

Matarajio katika mkutano wa BRICS nchini Afrika Kusini, Jumanne tarehe 22/2023
21 Aug 2023 12:14 - Kisali Shombe

Mkutano huo ambao utafanyikia Johannesburg nchini Afrika Kusini siku ya Jumanne, tarehe 22 Agosti 2023, unatarajiwa kuhu [ ... ]

Rais Ramaphosa Kuwa Mwenyeji wa Rais Xi Jinping wa China
21 Aug 2023 11:11 - Kisali Shombe

Rais Cyril Ramaphosa Jumanne ya tarehe 22 Agosti 2023, atakuwa mwenyeji wa Mheshimiwa Rais Xi Jinping wa China katika Zi [ ... ]

Other Articles

Social Media

Copyright © 2024 . Star Tv - Tanzania. All Rights Reserved.