Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Ummy Mwalimu ameagiza viongozi wawili kukamatwa na kusimamishwa kazi kwa kwenda kinyume na maagizo ya serikali.
Viongozi hao wawili ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyamlilio na mtendaji wa kijiji hicho wilayani Sengerema Mkoani Mwanza, ambao wamekutwa na madai ya kuwachangisha wananchi kwa nguvu fedha za maendeleo na ikiwa wanashindwa kutoa michangi viongozi hao hukamata mifugo yao.
Aidha, kufuatia malalamiko hayo, Waziri Ummy ameagiza watendaji wote wa vijiji na kata nchi nzima wasichangishe fedha kwa wananchi bila kibali kutoka kwa mkuu wa wilaya husika.
Mkazi wa Kijiji cha Nyamililo, Sijali Matihas amedai kuwa Machi 18 mwaka huu, mtendaji na mwenyekiti huyo walifika nyumbani kwake wakachukua mbuzi jike; "baada ya siku tano nilikwenda ofisi ya mtendaji na Sh30,000 kwa ajili ya kuchukua mbuzi wangu lakini kitendo kilichofanyika pale nilikosa amani"-Alibainisha Mathias.
Kwa upande wake mtendaji wa kijiji hicho Mariamu Mugunda amesema michango hiyo walikubalina na wananchi kupitia vikao vyote vya kijiji hicho na hajaenda kinyume na utaratibu.