Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza SACP. Ramadhani Ngh'anzi amethibisha kuwakamata viongozi 15 wa CHADEMA akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho taifa Freeman Mbowe.
Kamanda Ngh'anzi amesema Mwenyekiti huyo wa CHADEMA yupo Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano kufuatia kuwa na tuhuma nyingine katika mkoa huo.
"Baada ya kumkamata, wenzetu wa Dar es Salaam nao walitueleza kuwa wanamtafuta kwa makosa mengine anayodaiwa kuyafanya huko, hivyo tulimsafirisha kwenda Dar es Salaam anakoendelea kuhojiwa," - Amesema Kamanda Ng'anzi.
Aidha, Kamanda Ng'anzi amefafanua kuwa mara baada ya mahojiano yake na Jeshi la Polisi mkoani Dar es Salaam, atarejeshwa Mwanza ili aungane na wenzake wanaoshikiliwa kuhusiano na Kongamano la Katiba mpya ambalo hapo jana lilizuiliwa kufanyika.
Kamanda Ngh'anzi, amefafanua kuwa Mbowe alitiwa mbaroni alfajiri ya kuamkia jana Jumatano Julai 21 akiwa hoteli ya Kingdom mkoani humo, na kwamba viongozi wengine wa chama hicho wanaendelea kushikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Mwanza.