Star Tv

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema wakati umefika wa Wazanzibari kuungana pamoja katika vita dhidi ya usafirishaji na matumizi ya Dawa za kulevya pamoja na kuvitaka vyombo vya Ulinzi na Usalama kufanyakazi kwa weledi na ufanisi.

Dkt. Mwinyi ametoa rai hiyo leo katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya kupinga matumizi na Usafirishaji wa Dawa za Kulevya Duniani, hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul-wakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.

Amesema wakati Wazanzibari wanaungana na mataifa mengine Duniani kuadhimisha siku hiyo, wanapaswa kutambua kuwa kila mmoja ni muhanga wa atahri zitokazonazo na biashara hiyo haramu, kiafya, kiuchumi na kijamii.

“Matumizi ya dawa hizi za kulevya katika jamii husababisha kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu, kama vile wizi na unyang’anyi, matukio ya vifo, ajali, ugonjwa wa akili na kujamiiana, ulemavu pamoja na kuongezeka kwa umasikini…..zaidi ya yote biashara hii inachangia sana kutokuwepo kwa hali ya amani na utulivu katika jamii”- Amesema Rais Mwinyi

Amesema taarifa za matumizi ya dawa za kulevya kwa njia za kujidunga sindano, zinabainisha kuwepo wastani wa watu 3,200, wakati ambapo wataalamu wanaieleza hatua hiyo kuwa ni chanzo kikuu cha kuenea kwa kasi maradhi ya UKIMWI, virusi vya Homa ya Ini, maradhi ya Moyo, Figo pamoja na tatizo la ugonjwa wa akili.

Naye, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, ambae pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Kuratibu na Udhibiti Dawa za Kulevya, Hemed Suleiman Abdalla alisema mapendekezo ya kuibadili Tume hiyo na kuwa Mamlaka yanalenga kuleta ufanisi na kuiwezesha Zanzibar kuondokana na janga hilo na kusema kazi hiyo itawahusisha Wazanzibari wote.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti Dawa za Kulevya Kanali Burhan Nassor alisema kumekuwepo changamoto mbali mbali katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, hususas katika vyombo vya Ulinzi na Usalama, akitoa mfano wa Jeshi la Polisi ambapo mnamo mwaka 2018/19 jumla ya kesi 20 za makosa hayo zilifungwa na washtakiwa kuachiwa huru kutokana na sababu za Mkemia Mkuu kushidnwa kufika Mahakamani.

Alisema Idara ya Mahakama nayo imekuwa ikilalamikiwa kwa mamuzi yake, huku baadhi ya kesi zikionekana kutawaliwa na mazingira ya rushwa na uzembe, ukosefu wa maadili na kukosa nia thabiti ya kuiepusha nchi na janga hilo.

Katika hafla hiyo Viongozi mbalimbali wa Kitaifa walishiriki katika maadhimisho hayo, akiwemo Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Masoud Othman, Mawaziri, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa, Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama, Viongozi wa Dini pamoja na Viongozi wa Vyama vya Siasa.

Latest News

Mgogoro wa Maji unatishia Amani Duniani, inasema ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa...
21 Mar 2024 14:18 - Kisali Shombe

Siku ya Maji Duniani ambayo inafanyika tarehe 22 Machi ikiwa na kaulimbiu: 'Maji kwa Ustawi na Amani. Ambapo maji ni moj [ ... ]

Matarajio katika mkutano wa BRICS nchini Afrika Kusini, Jumanne tarehe 22/2023
21 Aug 2023 12:14 - Kisali Shombe

Mkutano huo ambao utafanyikia Johannesburg nchini Afrika Kusini siku ya Jumanne, tarehe 22 Agosti 2023, unatarajiwa kuhu [ ... ]

Rais Ramaphosa Kuwa Mwenyeji wa Rais Xi Jinping wa China
21 Aug 2023 11:11 - Kisali Shombe

Rais Cyril Ramaphosa Jumanne ya tarehe 22 Agosti 2023, atakuwa mwenyeji wa Mheshimiwa Rais Xi Jinping wa China katika Zi [ ... ]

Other Articles

Social Media

Copyright © 2024 . Star Tv - Tanzania. All Rights Reserved.