Marekani imetangaza kufikia makubaliano ya kupunguza ghasia kwa siku saba nchini Afghanistan ambayo inatumai yatawezesha kupatikana kwa mkataba wa amani na kundi la Taliban.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Mark Esper, ametangaza kufikiwa kwa makubaliano hayo baada ya mkutano wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO uliofanyika mjini Brussels, ikiwa ni siku moja baada ya Rais Ashraf Ghani wa Afganistan kusema kuwa mazungumzo kati ya Marekani na Taliban yamepiga hatua muhimu.
Esper amesema Marekani na kundi la Taliban zimejadiliana kuhusu pendekezo la siku saba la kupunguzwa kwa ghasia na kwamba leo wanashauriana na washirika kuhusu pendekezo hilo na kumekuwa na mikutano kuhusu mwelekeo utakaofuata.
Waziri huyo wa ulinzi wa Marekani hakusema ni lini hasa makubaliano hayo yataanza kutekelezwa, lakini afisa mmoja wa kundi la Taliban ameliambia shirika la habari la AFP kwamba kundi hilo litaanza kupunguza mashambulizi yanayotokana na shughuli zake za kijeshi kuanzia siku ya leo.
Mwisho.